DC: Leo niko hapa na rafiki yetu, Kevin Warnke. Kevin amekuwa akinisaidia kutafsiri maneno yangu mara nyingi hapa kwa KASSFM. Pia, alikuwa volunteer wa Peace Corps huko Kenya. Aliishi pwani, karibu na Malindi, na alikutana huko na msichana mrembo ambaye ni bibi yake leo. Wanaishi pamoja hapa DC. Kevin anafanya kazi kwa bunge kwa kumshauri mbunge mmoja kuhusu sera mbalimbali. Karibu Kevin.
KW: Asante Duncan. Nafurahi kuwa nanyi.
DC: Si kitambo, tulikuwa tunazungumza hapa kwa KASSFM kuhusu kifo cha mbunge mmoja hapa Amerika, Senata Kennedy, na jinsi alivyokuwa katika mstari wa mbele kwa wanasiasa hapa. Kabla ya kifo chake, Kennedy aliomba wanasiasa wabadilishe utaratibu wa kuchagua atakayemfuata. Je, huu utaratibu ukoje?
KW: Kuelewa utaratibu wenyewe, tunahitaji kukumbuka jinsi mfumo wa bunge letu ulivyoundwa. Hapa Amerika, tuko na bunge la juu, linalojulikana kama Senate, na bunge la chini, linaloitwa House of Representatives. Kwa House of Representatives, utaratibu ni wazi: kuna uchaguzi. Ni huo utaratibu unaotumika Kenya pia, kama "by-elections".
DC: Ndio. Lakini kwa viti vya Senate, wanafanya kivingine, si ndio?
KW: Kweli Duncan. Sharti, mila, na desturi za Senate zinachanganyisha hata Waamerika! Badala ya kulazimisha kuwe na uchaguzi, katiba yetu inasema kila jimbo litaamua jinsi ya kuchagua MaSenata wake. Katika jimbo lake Kennedy, linaloitwa Massachusetts, sheria inasema kama kuna nafasi wazi kwa viti vya MaSenata wake, kutakuwa na uchaguzi baada ya miezi mitatu. Kabla ya kifo chake, Kennedy aliomba serikali ya Massachusetts ibadilishe sheria kwa kumruhusu Governor kuteua mwakilishi wa muda kufanya kazi mpaka uchaguzi utafanyika.
DC: Kama kungekuwa na uchaguzi baada ya miezi mitatu, mbona Kennedy aliona ilikuwa muhimu kupata mwakilishi mwingine kwa huo muda mfupi?
KW:Kwa sababu ya namba moja yenye umuhimu mwingi katika Senate: Sitini. Kama MaSenata wanataka kufanya cho chote kwa Senate, inabidii kuwe na MaSenata sitini wanaokubali. Kuna MaSenata mia moja kwa ujumla--wawili kwa kila jimbo. Kama MaSenata arobaini na moja wanataka mswada fulani usiendelee, wanaweza kuusimamisha. Kennedy alipokuwa hai, WaDemokrat walikuwa sitini. Alipokufa, kukawa WaDemokrat hamsini na tisa tu, na ikawa vigumu kwa WaDemokrat kufanya wanavyotaka katika Senate.
DC: Na kama Senate inashindwa kufanya kazi yake, Rais Obama atashindwa kupitisha miswada na kubadilisha sharia za Amerika, si ndio?
KW: Ndio, ndio. Kama unavyojua, kubadilisha sheria hapa Amerika inabidii Senate na House of Representatives zote zipitishe mswada moja bila mabadiliko yoyote, na kwa Rais kuukubali hivyo hivyo.
DC: Nilisoma historia ya Kenya kidogo na nilishangaa kuona hata Kenya ilikuwa na Senate na House of Representatives kwa miaka michache. Na hata katika Katiba Bomas ya miaka mitano iliyopita, wengine walipendekeza kuwe na Senate tena. Pengine unaweza kutushauri na uzuri na ubaya wa bunge hilo.
KW: Kwanza, tukumbuke sababu ya kuwa na mfumo wetu hapa Amerika. Wakati wa ukoloni, Amerika haikuwa koloni moja, ila makoloni kumi na tatu. Makoloni haya yaliungana wakati wa vita kupigania uhuru kutoka kwa utawala wa Uingereza. Baada ya kupata uhuru, viongozi wa makoloni haya waliona bora waungane. Kama WaSwahili wasemavyo, "Kidole kimoja hakivunji chawa". Wakati ule, chawa yetu ilikuwa Uingereza. Lakini kuungana na kuanzisha serikali ya taifa ilileta swala nyeti kuhusu jinsi ya kuwakilisha wananchi. Kabla ya kuungana kila koloni lilikuwa na serikali yake.
DC: Na viongozi wa majimbo yenye watu wachache walitaka kila jimbo liwakilishwe kwa usawa. Viongozi wa majimbo yenye watu wengi walitaka kuwakilishwa kulingana na namba ya wananchi wanaoishi kwa jimbo lenyewe. Baada ya mvutano baina ya majimbo, waliafikiana kwamba kutakuwa na bunge moja kutetea maoni ya majimbo, ambalo ni Senate, na bunge moja kutetea maoni ya watu wenyewe, ambalo ni House of Representatives.
KW: Ndio. Na tukiangalia maandishi ya wale ambao waliafikiana hivyo, kazi ya Senate ilikuwa kuhakikisha miswada ya House of Representatives ilikuwa mizuri. Inasemakana Rais wetu wa kwanza, George Washington, alisema kazi ya Senate ilikuwa "kupoza" miswada kama kisahani kinavyotumika kupoza chai moto.
DC: Unaona hii ni kweli? Senate "hupoza" miswada?
KW: Bila shaka. House of Representatives hufanya kazi yake kivingine kabisa. Bunge hili linaongozwa na uongozi wa chama kimoja. Kupitisha mswada kunahitaji zaidi ya asilimia hamsini ya wabunge wake. Hii ni sawa na bunge ya Kenya. Miswada ikipita House of Representatives, huenda na kukaa kwa muda mrefu kwa Senate. Wengine wanasema ndio vizuri. Inazuia miswada mibaya isipite bila kuangaliwa sana na kuwe na watu wengi wanaoona inafaa.
DC: Lakini wengine wanasema ni vibaya kwa sababu MaSenata wanaowakilisha majimbo yenye watu wachache wanaweza kuzuia Rais na chama chake, hata ikiwa wanapendwa sana na wananchi.
KW: Kweli. Wakati Bush alikuwa Rais, WaRepublican walilalamikia MaSenata WaDemokrat kwa kuwazuia. Vile vile, leo WaDemokrat wanalalimikia MaSenata WaRepublican. Kwa hiyo, ubaya wake ni kwamba kama Rais na chama chake, hata kama wanawakilisha maeneo yenye watu wengi sana, hata kama wananchi wengi wanawakubali na kukubali na mapendekezo au miswada yao, hata kama haya yote ni kweli, kama MaSenata arobaini na mmoja hawataki (wengi wao kutoka majimbo yenye watu wachache), ni bas. Haitafanyika.
DC: Si hii inafanya iwe vigumu kupitisha miswada?
KW: Ndio. Uzuri wake ni kwamba hata kama, kwa mfano, jimbo moja halipendwi, eneo lake ni dogo, na falsafa ya watu wake ni tofauti, wakilishi wake watakuwa na nguvu kutetea matakwa yao.
DC: Kevin, Asante kwa kuja kutuelezea hayo yote.
KW: Asante. Nimefurahi kuzungumza nanyi.
Kevin's Shared Items
Saturday, October 24, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment